Home » » Usafi tuliomuonyesha Obama udumishwe

Usafi tuliomuonyesha Obama udumishwe

Written By Unknown on Saturday, July 6, 2013 | 01:08


Kwa takribani wiki moja iliyopita wakazi wa jiji la Dar es Salaam walishuhudia mji wao ukiwa msafi kama ambavyo uliwahi kuwa huko nyuma kati ya mwaka 1996-2000 halmashauri ya ya Jiji la Dar es Salaam ilipovunjwa baada ya kushindwa kukidhi vigezo vyote vya uwajibikaji hasa eneo la usafi, na badala yake ikaundwa Tume ya Jiji iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Charles Keenja.

Usafi huu ulishuhudiwa kila kona, hasa kwenye barabara kuu na mitaa ya katikati ya Jiji. Tumeshuhudia msako mkali wa wachuuzi maarufu kama wamachinga; tumeona mama lishe na baba lishe nao wakifurushwa sehemu mbalimbali ambazo kimsingi siyo za kufanya biashara.

Operesheni hii ilikuwa nzito. Polisi waliobeba silaha walikuwa nyuma ya askari mgambo waliokuwa wanapita kila mtaa wakivunja meza za wachuuzi, wakivunja vibanda vyao na kuondoka na bidhaa zilizokuwa zinauzwa; kuna maeneo baadhi ya wachuuzi walikamatwa.

Ilikuwa ni wiki ya mikikimikiki ili kufanikisha kazi ya kuliweka Jiji hilo katika hali ya usafi ili ugeni mkubwa wa Rais Barack Obama, amabo uliingia nchini juzi na kuondoka jana, usikutane na hali ya kutufedhehesha, uchafu. Uchafu ni aibu, siyo sifa njema.

Kwa kujua ukweli huo kwamba uchuuzi wa ovyo ovyo kila mahali, kila kona unachangia kuchafua Jiji, na kwa kuelewa kwamba kote walikotanda wachuuzi waliofurushwa hawaruhusiwi kisheria, basi manispaa zote za Dar es Salaam, kuanzia Temeke, Ilala hadi Kinondoni zikaendesha operesheni kabambe ya kusafisha maeneo yao.

Tunashukuru kwamba operesheni hii walau umetusetiri na aibu mbele ya ugeni huu mkubwa ambao umetujengea jina zuri kimataifa kwamba Tanzania ipo na inavuma. Ziara ya Obama imeacha mengi, lakini kubwa ambalo halina ubishi ni ukweli kwamba imeitangaza Tanzania kila kona ya dunia hii. Ni bango kubwa la kibiashara, la kuvutia wawekezaji, la kuweka wazi kwamba tupo na tunakubalika kimataifa.

Kwa hiyo, wenye mamlaka katika manispaa hizi tatu wamejua vilivyo kwamba walikuwa na wajibu wa kutimiza wajibu wao walau kwa muda wa wiki moja tu ili maeneo yetu yawe safi; kwamba ilifika mahali siyo tu barabara ambazo tumezoea kuona kina mama waliochoka wakifagia kwa kutumia zana duni mno, yalipatikana magari ya kufagia, yalipatikana magari ya kumwaga maji barabarani, lakini pia yalipatikana ya kusugua lami (kudeki) ili ing’ae isituaibishe.

Viongozi wetu wanasafiri sana nje. Wakifika kwenye miji ya wenzetu huko nje, wanajionea wenyewe kwanza ilivyopangwa, pili ilivyo safi. Usafi ni mojawapo ya sifa muhimu kwa kila mji, wanaochaguliwa kwenye miji hii wakiomba kura kwa wananchi wao pamoja na mambo mengine wanayoahidi ni kuendeleza sifa njema ya kuwa na mazingira bora ya kuishi. 

Yaani kuhakikisha taka ngumu na za vimiminika zinaondolewa kwenye makazi ya watu, kuhakikisha kwamba barabara bora zaidi zinajengwa na zilizopo zinatunzwa, lakini la umuhimu zaidi kuwahakikishia wakazi wa miji hiyo usalama wa afya zao wakati wote.

Tanzania siyo kisiwa, miji yake yote ukiwamo Dar es Salaam unapashwa kuwa msafi, ivutie wageni, ivutie na kuwapa amani wakazi wake, ipangwe ili kuepuka kero mbalimbali za misongamano isiyokuwa ya lazima; kwa bahati mbaya kinyume chake ndiyo uweli wa mambo. Ukweli huu siyo wa bahati mbaya ni wa kujitakia, ni wa makusudi ni wa kufumbia macho sheria zikivunjwa. 

Ni wa kubembeleza kura kwa njia ya ovyo kabisa ambayo haileti ustawi wa nchi hata kidogo.

Hakuna asiyekumbuka kwamba wakati Jiji la Dar es Salaam mwaka 1996 linavyunjwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye, wamachinga walikuwa wametanda kila kona, walikuwa wamekuwa na ujasiri wa kujenga hata vibanda vya kuuza bidhaa ndogo ndogo na hata mitumba karibu kabisa na lango la Ikulu.

Eneo ambalo linajulikana kama eneo kuu la biashara la mjini kati (central business district – CBD) lilikuwa limejaa vibanda vya mbao vilivyojengwa ovyo ovyo. Kila upenyo ulizibwa, kisa uchuuzi; maeneo yote ya waenda kwa miguu yaligeuzwa kuwa sehemu ya kupanga bidhaa za wamachinga. Tume ilisafisha ghasia yote hii na kuacha jiji liking’aa.

Leo miaka 17 baadaye tumerudi kwenye tabu ile ile. Uchuuzi kila mahali; wamachinga wanatawala; barabara nzuri zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa na kuwekwa sehemu ya waenda kwa miguu imegeuzwa uwanja wa bidhaa za wamachinga, uchuuzi huu inafanyika mchana na usiku, wenye mamlaka yao wapo na wanaona. 

Hawafanyi kitu. Kisa? Wanabembeleza kura!
Ziara ya Obama kwa mara nyingine tena imetukumbusha kwamba mjini mazingira yake yanapaswa kuwa masafi, shughuli zote mjini zinafanywa kwa mujibu wa sheria na kanuni za mipango miji. 

Ziara ya Obama walau kwa wiki moja imetukumbusha kwamba kumbe bado manispaa hizi zina askari mgambo wenye wajibu wa kusimamia sheria ndogondogo zilizotungwa pamoja na mambo mengine kuweka utaratibu wa kuendesha shughuli mjini.

Tunatamani sana kwamba baada ya Obama kuodoka jana na kwa baada ya Watanzania kumuonyesha ukaribu mkubwa kwamba ni watu wa amani na watulivu, sasa hali hii ya usafi itadumishwa.


Na Mhariri Nipashe
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. harod tz - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger