Ndugu zangu huu ndiyo ukweli ulivyo. Familia ikiwa yenye migogoro, maendeleo yatakuwa ni ndoto. Ndiyo maana tunajifunza mapenzi kila kukicha.
Katika matoleo yaliyopita, nilianza kwa kueleza kuhusu wale ambao wanarukia mapenzi bila kuwa na uhakika na hisia zao, mwishowe wanaumia au wanaumizwa!
Mwenzako anawekeza kwako akiamini yupo na mtu sahihi, kumbe kichwani mwako unamfanya daraja. Sawa, acha awe daraja na akuvushe salama, vipi moyoni mwake? Unajua anawaza nini?
Unajua mwisho wa fikra zake katika maumivu ya mapenzi? Unajua maamuzi ambayo anaweza kuyachukua? Kwa hakika kila kitu ni giza maana huwezi kuingia ndani ya moyo wa mwenzako na kujua kile anachowaza.
Tuendelee kujifunza.
ACHA MAPENZI YA KUIGIZA
Wapo wanaoingia kwenye uhusiano hata kama hawana lengo la kuwachuna wenzao lakini hawana uhakika na hisia zao. Wanaamua kujaribu kuona kama labda baadaye wanaweza kupenda.
Kutokana na hilo basi, kinachofuata inakuwa ni kufanya maigizo tu na si kweli kwamba wapo kwenye uhusiano ‘seriously’. Hili ni tatizo.
Wapo wenzangu na miye wanaojiita marioo, wanajiingiza hata kwa majimama ili wapate fedha, siyo sawa. Hutaona athari zake haraka, lakini ukweli ni kwamba unajiweka katika nafasi ya kupoteza hisia za kupenda hapo baadaye.
NI HISIA TAMU ZENYE CHUNGU
Utamu wa mapenzi unakuja pale wawili wanapokutana wakiwa na hisia sawa. Uchungu hutokea pale ambapo mmoja anajua kwamba yupo kwenye uhusiano ulio sahihi wakati mwingine akiwa na uhakika kuwa anazuga tu kwa muda,
Kumbuka hapo tayari kunakuwa na hisia mbili tofauti zinazosafiri pamoja. Moja inakuza upendo, nyingine inakuza chuki. Unajua mwisho wake? Ni kama nilivyoeleza kwenye kipengele kilichopita.
KUTOKA KWANGU
Ya nini yote hayo? Hebu simama kwa miguu yako miwili. Acha kucheza na hisia za mwingine. Heshimu moyo wa mwenzako kama unavyoubembeleza wako.
Acha kumpotezea muda mwenzako. Usiingie kwenye uhusiano kwa sababu ya kitu maana ipo siku inaweza kukutokea puani.
Kama wewe huna nia ya kupenda au kupendwa, waache wenzako wenye lengo hilo, wewe uendelee na mambo yako huko chochoroni, tena uwe wazi, kuwa upo kazini!
Post a Comment