(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo ni “kuwa na taifa lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye
uwezo na malezi bora, linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri
katika michezo ifikapo mwaka 2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni
‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa kuwezesha upatikanaji mzuri wa
habari, kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza utamaduni na michezo kwa
umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali hii ya CCM
imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya
kisera ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii,
Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya
matendo ya watawala. Tanzania imegeuka kuwa taifa linalofungia magazeti
yanayofichua ufisadi, uchafu na matumizi mabaya ya madaraka miongoni mwa
viongozi, watendaji na watumishi wa Serikali hii ya CCM. Tanzania
imegeuka, chini ya usimamizi wa Wizara na Serikali hii ya CCM, kuwa
taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno,
kuwatoboa macho, kuwamwagia tindikali na hata kuwaua. Tanzania sio nchi
inayoandaa vijana wake tena. Haiwapi tena elimu bora wala kuwapatia
maarifa, uwezo na malezi bora; ni nchi isiyowawezesha wala kuwathamini
vijana wake; ni nchi inayoruhusu vijana wake kunyonywa na kutoendelezwa;
na ni taifa ambalo limeachia utamaduni utambulisho wake kama taifa
kupotea kabisa. Aidha, katika fani ya michezo ya aina zote, Tanzania
imeporomoka kutoka taifa lililokuwa linaheshimika kimataifa katika miaka
ya sabini na kuwa alichokiita rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, ‘kichwa
cha mwendawazimu’ ambacho kila kinyozi anajifunzia kunyolea!
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaarifu
Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya
fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni
taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao
kwa taifa na kama ajira yao. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda
Waandishi wa Habari Ulimwenguni (the Committee to Protect Journalists -
CPJ) iliyotolewa mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa
CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni
hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao kutokana na hatari ya
kuuwawa kwa mwaka 2012 (20 Deadliest Countries in 2012). Kwa mujibu wa
taarifa hiyo, ilishikilia nafasi ya 7 ulimwenguni kati ya nchi 20
zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa habari
duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa maisha. Aidha,
Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa
mauaji ya waandishi wa habari. Kwa mujibu wa takwimu za CPJ, kati ya
waandishi waliouwawa mwaka 2012, karibu ya 20% waliuwawa ama na maafisa
wa serikali au na majeshi yake. Karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa
habari waliuawa kwa sababu ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za
hatari. Taarifa hiyo inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili 2013,
waandishi wa habari wapatao 30 tayari wamekwishauawa ulimwenguni wakati
wakitimiza wajibu wao; wakati mwaka 2012 waandishi wa habari 103
waliuwawa ulimwenguni kote.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya
CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi yanayodhihirisha kwamba
maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yako hatarini kutokana na
vitendo na vitisho kutoka kwa Serikali na watendaji wake ambao hawataki
kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa hadharani. Kudhihirisha kauli hii
tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja wa wahanga wa vita dhidi
ya wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa
na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita ‘kupinga
mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na kudai kwamba alikuwa Mkenya
na ‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda
wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai
kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa!
Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu
mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi
Mkuu, katika eneo la Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani
Mwanza, mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu
wapatao 15 waliojiita “Green Guard” - wa “chama cha kijani.” Katika
“kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi
mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa anawaandika ‘vibaya’ Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu
alikutwa amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari
viliripoti kuwa macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina
ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya
habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa
gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa
kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo
Cross Park katika eneo la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya
mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji
cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.Ngumba alikuwa
mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi uliopita Machi,
mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam, anaishi kwa
wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na ‘ofisa usalama’ kwa
kile kilichoitwa ‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa
aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga cha ITV, John Lubungo
ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari zinazohusu wafanyabiashara
au biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo inadaiwa kufanywa na watu
wakubwa nchini, wakiwemo vigogo serikalini. Kuna orodha ndefu ya
waandishi wa habari waliotishwa na wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na
polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es Salaama) kwa tuhuma
mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa kufuatiliwa na watu
wasiowafahamu.”
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda
kujikweza, Mzee Tegambwage hakutaja shambulio la tindikali na mapanga
dhidi yake na mwandishi mwenzake Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi,
ambalo baadae lilifungiwa na Serikali hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na
Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio
kwa maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi
yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejeaRipoti ya Timu Maalum ya
Uchunguzi Iliyoteuliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) Kuchunguza Mazingira Yaliyopelekea Kuuawa kwa
Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 Katika Kijiji cha
Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa, iliyotolewa na Baraza la
Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), taasisi
mbili huru zinazojihusisha na masuala ya habari Tanzania.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “...
yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha
waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za
CHADEMA katika kijiji cha Nyololo. Zaidi ya hapo, Daudi Mwangosi
mwenyewe aliuawa akiwa mikononi mwa polisi huku wakisimamiwa moja kwa
moja na Kamanda (wa Polisi wa Mkoa wa Iringa SACP Michael) Kamuhanda.”
Ripoti hiyo inaelezea jinsi Marehemu Mwangosi alivyouawa: “Alipoangalia
nyuma, Daudi Mwangosi aliona kikundi cha polisi wakimpiga mwandishi mkuu
wa gazeti la Nipashe wa Iringa, Godfrey Mushi.... Wakati mwandishi
Godfrey Mushi akiwa bado anapigwa na polisi, marehemu Mwangosi
aliwakimbilia akiwaomba waache kumdhuru zaidi Mushi kwa kuwa alikuwa
mwandishi tu. Polisi hawakumsikiliza. Badala yake wakamburuta mwandishi
huyo ambaye tayari alikuwa amepoteza fahamu na kumweka kwenye gari lao
na wakamgeukia Daudi Mwangosi mwenyewe, wakampiga kwa nguvu mpaka
akapoteza fahamu.”
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi
Mafinga Mwampamba kuwataka askari polisi waache kumpiga marehemu
Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi
alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye kumwangukia miguuni mwake kuepuka
kipigo zaidi.” Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, “picha za mgando
zinaonyesha polisi mmoja akipiga bomu la machozi tumboni mwa marehemu
Mwangosi kwa karibu kabisa.” Bomu hilo liliusambaratisha mwili wa
marehemu Mwangosi aliyekufa papo hapo. Kwa sababu marehemu Mwangosi
alikuwa chini ya miguu ya OCS Mwampamba, “naye pia alijeruhiwa vibaya.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu Mwangosi.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea
Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo,
iliyobaini kwamba Marehemu Mwangosi “... alizingirwa na askari, aliteswa
na hatimaye ... alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa mujibu wa
Taarifa hiyo, “... Tume imejiridhisha kuwa tukio la lililopelekea kifo
cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.” Taarifa ya Tume inafafanua kuwa,
“... Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki ... ya
kuishi, haki ya kutoteswa na kupigwa, haki ya usawa mbele ya sheria na
haki ya kukusanyika na kutoa maoni.”
Mheshimiwa Spika,
Siku moja baada ya mauaji ya Daudi
Mwangosi, Jeshi la Polisi lilianza kampeni kubwa ya kujaribu kuficha
ukweli juu ya kuhusika kwake, kwa kuhamishia lawama kwa watu wengine
wasiohusika na mauaji hayo. Kwa mfano, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na
vyombo vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na
kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata
Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba
baada ya ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa
polisi na “kitu kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo
na kumlipua Mwangosi.”
Njama hizi za kuficha ukweli zimeumbuliwa na
Ripoti ya MCT/TEF inayobainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini
ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia
imeelezea kwa kirefu jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa
zinazokinzana juu ya kuhusika kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa
mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi
alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu la machozi
ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea
kwenye televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia
lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua
Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Hata Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi,
iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuongozwa
na Jaji Stephen Ihema imethibitisha kuhusika kwa Jeshi la Polisi na
mauaji ya Marehemu Mwangosi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu
kulisafisha Jeshi la Polisi kutoka kwenye lawama ya kumuua Marehemu
Mwangosi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa
kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu
waogope na kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo inakiri kwamba “hapakuwepo
umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji
tayari askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi
hiyo, “… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na
kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM na Jeshi la Polisi
wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika
zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi. Kwa mfano,
Ripoti ya MCT/TEF inaashiria kuwa sababu ya Marehemu Mwangosi kuuawa ni
kwamba yeye “... ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC (Kamuhanda)
‘maswali magumu’ kiasi cha kumkera kiongozi huyo wa jeshi la polisi.”
Ripoti hiyo inafafanua kwamba “baada ya mkutano huo na waandishi, ...
baadhi ya polisi ... waliwaonya wasiende Nyololo kwa ajili ya kukusanya
habari za shughuli za kisiasa za CHADEMA kutokana na uwezekano wa
kutokea kwa hali hatarishi.” Aidha, “baada ya mkutano wa waandishi wa
habari wa asubuhi katika ofisi za RPC (Kamuhanda), ... askari mmoja
mpelelezi alimfuata Mwangosi na kumwambia: ‘Ina maana gani kwenda
Nyololo kuandika habari za Chadema ambazo zinaweza kuishia na kifo
chako?’” Vile vile, Ripoti ya MCT/TEF inabainisha, ni “... wazi kwamba
Polisi walikuwa wanawawinda waandishi wa Iringa ambao walikuwa
wakiwajua.”
Mheshimiwa Spika,
Siku tatu baada
ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
katika Jeshi la Polisi Robert Manumba alitoa kauli kwa vyombo vya habari
kuhusu matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari ambapo alisema
“….matukio ya aina hii yapo na yataendelea kuwepo.” Katika kuthibitisha
kwamba Serikali hii ya CCM ina sera isiyo rasmi ya kulenga kuwadhuru
waandishi wa habari wanaowaandika watawala vibaya na hata kuwaua, kauli
ya DCI Manumba imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulongo
wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu jijini Arusha. Kwa mujibu wa
vyombo vya habari, Mkuu huyo wa Mkoa aliwatahadharisha waandishi kwa
kuwaambia kwamba “unapoingia katika mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa
Serikali unaiweka roho yako rehani…. Kuweni makini.”
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake kwenye mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyaita matamshi ya DCI Manumba na Mkuu wa
Mkoa Mulongo kuwa ni ‘matendo ya kigaidi’ kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia
Ugaidi, 2002, ambayo inafafanua ‘matendo ya kigaidi’ kuwa ni pamoja na
vitisho vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au majeraha makubwa
kimwili, kuhatarisha maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa umma
ambavyo vimelengwa au ambavyo kwa hulka au muktadha wake vinaonekana
vimelengwa kutishia umma au sehemu ya umma.
Kwa mara nyingine
tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi
mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hiyo ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi
ni sahihi au la. Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka
kujua ni kwa nini DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo bado hawajakamatwa
na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi hadi sasa? Kama tafsiri hiyo sio
sahihi, basi Serikali hii ya CCM itamke mbele ya Bunge lako tukufu
kwamba ni sera yake rasmi kwamba waandishi wa habari wanaoiandika
Serikali au viongozi wake vibaya ‘wanaweka roho zao rehani’!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ambazo zimetolewa na Serikali hii ya CCM ndani ya Bunge lako
tukufu zinathibitisha kuhusika kwa Serikali katika, kama sio kupanga
basi angalau kubariki, mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama vya
Serikali kwa waandishi. Na moja ya kauli za Serikali ambazo
zimeifadhaisha na kuisikitisha sana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni
ile iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Mh. William Lukuvi pale alipomsifu
Kamanda Kamuhanda wakati wa mjadala wa Wizara ya Mambo ya Ndani: “Katika
kitabu hiki cha Kambi ya Upinzani, wamekutaja sana (Kamuhanda),
hawawezi kukupongeza. Huko Iringa Kamanda unafanya kazi nzuri sana,
usitetereke na makamanda wako wa huko Iringa.”
Ikumbukwe, Mheshimiwa Spika,
kwamba mtu anayesifiwa kwa ‘kufanya kazi nzuri sana kule Iringa’ ni
yule yule ambaye aliyelaumiwa na Tume ya Haki za Binadamu – ambayo
Makamishna wake wote ni wateule wa Rais kwa mujibu wa Katiba – kuwa
alikiuka sheria za nchi yetu na misingi ya utawala bora kufuatia tukio
la mauaji ya Marehemu Mwangosi! Mtu anayeshauriwa na Waziri Lukuvi
kwamba ‘asitetereke’ ni yule yule ambaye MCT/TEF imemhusisha na
usimamizi wa moja kwa moja wa mauaji ya Mwangosi. Needless to say, mtu huyu bado yuko huru na hajachukuliwa hatua yoyote licha ya mshangao mkubwa kitaifa na kimataifa!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi
mbele ya Bunge lako tukufu kama kauli ya Mheshimiwa Lukuvi kuhusu
kuhusika kwa Kamanda Kamuhanda na Jeshi la Polisi katika mauaji ya
Marehemu Mwangosi ndio msimamo rasmi wa Serikali hii ya CCM. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kuliambia
Bunge lako tukufu ni nini msimamo wake rasmi juu ya Taarifa ya Tume ya
Haki za Binadamu na Ripoti ya MCT/TEF kuhusu kuhusika kwa Jeshi la
Polisi na Kamanda Kamuhanda katika mauaji ya Marehemu Mwangosi. Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimya cha Serikali hii ya CCM
juu ya maswali haya muhimu ni ushahidi dhahiri kuwa mauaji haya ni
sehemu ya mkakati ulioasisiwa na Serikali hii ya CCM wa kuwanyamazisha
waandishi wa habari kwa nia moja tu: kufifisha uhuru wa kupata na kutoa
habari muhimu zinazohusika kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Miezi
sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daudi Mwangosi, mwandishi mwingine
mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom
Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake baada ya
nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa kuwa
watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Badala ya
kuchukua hatua za dhati kuwachunguza na kuwakamata wale wote waliohusika
na tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na Idara ya
Usalama wa Taifa, maafisa waandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu na
viongozi waandamizi wa CCM chini ya Naibu Katibu Mkuu wake Mheshimiwa
Mwigulu Nchemba na baadhi ya waandishi habari maslahi, walianzisha
kampeni kubwa ya kuipakazia CHADEMA na Mkurugenzi wake wa Ulinzi na
Usalama Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi kutokana na
ushahidi wa kutunga!
Mheshimiwa Spika,
Kwa
vile njama dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare zimegonga mwamba baada ya
Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali mashtaka ya ugaidi dhidi
yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa
taarifa rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya waliohusika na jaribio
la kumuua Bw. Kibanda. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya
kuhusika kwa Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu na CCM
katika kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare
ili kuwapumbaza Watanzania wasihoji shambulio la kigaidi dhidi ya Bw.
Kibanda.
Kutoa taarifa ya uongo kwa lengo la kuanzisha
mashtaka ya jinai mahakamani au kutengeneza ushahidi wa uongo kwa lengo
la kuipotosha mahakama ni makosa ya jinai yenye adhabu ya kifungo cha
miaka saba kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu ya Tanzania. Ni muhimu
kwa ukweli wa jambo hili kujulikana sio tu kwa ajili ya kuwawajibisha
kijinai wahusika, bali pia kwa lengo la kulinda demokrasia na utawala wa
sheria katika nchi yetu. Kama alivyosema Chris Conybeare, Katibu Mkuu
wa Chama cha Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) katika ujumbe wake kwa
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dk. Fenella
Mukangara juu ya mauaji ya Marehemu Mwangosi: “Waandishi wa habari
wanapouawa demokrasia pia inakufa.”
3. MAELEZO NA UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Idara ya Habari (MAELEZO) ilikasimiwa majukumu na mali za lililokuwa
Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na Sheria ya Kufuta Shirika la
Habari la Tanzania, Na. 7 ya mwaka 2000. Wakati SHIHATA ilikuwa na
ukiritimba wa kukusanya habari pamoja na mamlaka ya kusajili waandishi
wa habari, ukiritimba huo na mamlaka ya usajili wa waandishi wa habari
yalifutwa kabisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, 1991 (‘Tume ya Nyalali’), iliyobaini kwamba Sheria ya SHIHATA ilikuwa inakiuka misingi ya uhuru wa mawazo na uhuru wa habari.
Kwa sababu hiyo, majukumu mapya ya Idara ya Habari, kama
yalivyofafanuliwa katika kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Kufuta SHIHATA,
ni pamoja na kutoa, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji na uendeshaji
wa za kukusanyia na kusambaza habari; kukusanya na kusambaza habari na
kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu usambazaji habari na
utendaji wa mashirika ya habari. Idara ina ofisi katika baadhi ya mikoa
ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti na
SHIHATA, Idara ya Habari haina na haijawahi kupewa jukumu la kisheria
la kuwa msimamizi wa vyombo vya habari na wanahabari nchini. Hata hivyo,
kama ilivyokuwa kwa SHIHATA, Idara hii imekuwa inawauzia waandishi wa
habari vitambulisho (press cards) ambavyo vimekuwa vinatumika kama
vitambulisho cha kazi kwa waandishi wa habari hapa nchini. Vitambulisho
hivyo vimekuwa vinauzwa kwa shilingi za Tanzania elfu ishirini, lakini
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba bei ya vitambulisho
hivyo imepanda mwaka huu hadi kufikia shilingi elfu thelathini. Aidha,
vitambulisho hivyo hutolewa kila mwaka katika Ofisi za MAELEZO Dar es
Salaam na hivyo kusababisha gharama na usumbufu mkubwa kwa waandishi wa
habari walioko mikoani.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi vya Idara ya Habari ni kinyume cha Sheria ya Kufuta
SHIHATA. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu Idara ya
Habari imetoa wapi mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa
kuwalazimisha kununua vitambulisho vya uandishi habari. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya
Bunge lako tukufu kama kuna masharti yoyote ya kisheria yanayolazimu
waandishi wa habari wasajiliwe na MAELEZO kwa kupatiwa vitambulisho vya
kazi na Idara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu
kwamba Idara ya Habari imejitwalia mamlaka ya kusajili waandishi wa
habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya taaluma yao, lakini
pia imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa kupanuka kwa demokrasia na uhuru
wa habari katika nchi yetu. Historia yake inaanzia miaka ya mwanzo ya
utawala wa kikoloni wa Kiingereza wakati walipotunga Sheria ya Magazeti
ya 1928. Chini ya Sheria hiyo, wakoloni walidhibiti ukuaji wa vyombo vya
habari vya wenyeji wa Kiafrika kwa kuviwekea masharti ya kusajiliwa
baada ya kutoa dhamana ya fedha taslimu.
Marekebisho ya Sheria
hiyo yaliyofanywa mwaka 1952 yaliweka masharti magumu zaidi ya usajili
wa magazeti pamoja na kuongeza kiwango cha dhamana kutoka pauni za
Kiingereza 160 hadi pauni 520. Kwa mujibu wa Martin Sturmer katika
kitabu chake The Media History of Tanzania, wakati magazeti ya
Wamisionari na yale yaliyokuwa yanaunga mkono sera za utawala wa
kikoloni katika Tanganyika hayakudaiwa kulipa dhamana, magazeti
yaliyokuwa na mrengo wa upinzani wa sera za dola ya kikoloni
yalilazimika kulipa dhamana hiyo.
Baadae mwaka 1955 dola ya
kikoloni iliongeza udhibiti zaidi wa vyombo vya habari kwa kuingiza
katika Sheria ya Adhabu vifungu vipya vilivyokataza uchapishaji wa jambo
au taarifa yoyote lenye uwezo wa kuleta chuki dhidi ya serikali ya
kikoloni au watendaji wake. Kama anavyosema Sturmer, kutokea hapo sheria
hiyo ya uchochezi ndio imekuwa kizingiti kikubwa kwa uhuru wa magazeti
katika Tanzania. Haiwezi kuwa ajabu kwamba wahanga wa kwanza wa sheria
hiyo ya uchochezi walikuwa mabwana Kheri Rashidi Baghdelleh na Robert
Moses Makange waliokuwa wahariri wa gazeti la Mwafrika; na mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU aliyejulikana kama Julius Kambarage Nyerere!
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha ajabu ni kwamba sheria iliyotungwa na wakoloni wa Kiingereza
kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji wa Kiafrika wasidai uhuru au kuanika
uchafu na uonevu wa dola ya kikoloni haikufutwa mara baada ya uhuru.
Badala yake, sera za habari za dola ya uhuru sio tu zilipokea na
kuzidisha masharti ya kisheria dhidi ya uhuru wa habari kwa kutunga Sheria ya Magazeti
ya mwaka 1976 iliyoongeza makali ya sheria ya uchochezi, bali pia
zilitaifisha magazeti na vyombo vingine vya habari binafsi vilivyokuwepo
wakati wa uhuru.
Hivyo, kwa mfano, Shirika la Utangazaji la
Tanganyika (TBC) lilitaifishwa kwa Sheria ya Bunge ya tarehe 16 Machi
1965 na kubatizwa jina jipya la Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Aidha, tarehe 5 Februari, 1970, gazeti binafsi la The Standard lilitaifishwa na Serikali. Na ilipofika tarehe 26 Aprili, 1972, The Daily News,
gazeti jipya la Serikali lilianzishwa kwa kuunganisha The Standard na
gazeti la The Nationalist lililokuwa linamilikiwa na TANU. Hivyo basi,
kama anavyosema Sturmer katika historia yake ya vyombo vya habari
Tanzania, “kufikia mwaka 1976 Serikali ya Nyerere ilishafanikisha lengo
lake kuu la sera ya habari – kuwa na udhibiti juu ya vyombo vyote vikuu
vya habari....”
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu huu wa udhibiti juu ya vyombo vya habari kwa kutumia Sheria ya Magazeti
ulishambuliwa na Tume ya Nyalali kwa kukiuka matakwa ya ibara ya 18 ya
Katiba inayotoa uhuru wa mawazo na uhuru wa habari. Kwa maneno ya Tume
hiyo, Serikali inakiuka uhuru wa mawazo na wa habari “... kwa
kujihusisha na kuchuja habari zinazotolewa kwa wananchi.” Tume
ilipendekeza marekebisho makubwa katika Sheria ya Magazeti “... ili
kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa habari na wa mawazo na kulegeza uchujaji
wa habari.” Mapendekezo haya ya Tume ya Nyalali hayajatekelezwa hadi leo
hii, zaidi ya miaka ishirini na mbili tangu Tume hiyo iwasilishe
Taarifa yake kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tanzania imebakia mateka wa sera za habari za kikoloni na za
utawala wa kiimla wa chama kimoja, jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu
wa Zimbabwe wamepiga hatua kubwa katika kupanua uhuru wa habari. Hivyo,
kwa mfano, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopitishwa kwa kura ya
maoni ya wananchi wa nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu inatoa uhuru wa
mawazo ambao unajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo
na habari nyingine; uhuru wa mawazo ya kisanii na wa utafiti wa
kisayansi na uhuru wa taaluma.
Aidha, Katiba hiyo inatoa uhuru
wa habari ambao ni pamoja na ulinzi wa vyanzo vya habari vya waandishi
wa habari; na uhuru wa uanzishaji wa vyombo vya utangazaji ambavyo
havitakiwi kuwa chini ya udhibiti wa serikali au maslahi ya kisiasa au
kibishara. Vile vile, Katiba Mpya ya Zimbabwe inavilazimu vyombo vya
habari vinavyomilikiwa na Serikali kuwa huru kuamua mambo gani ya
kutangaza; kutokupendelea na kutoa fursa sawa kwa ajili ya kutangaza
maoni tofauti na mawazo yanayokinzana.
Mheshimiwa Spika,
Katiba Mpya ya Zimbabwe inatoa pia uhuru wa taarifa (access to
information). Hivyo, kwa mfano, kila raia au mkazi wa kudumu wa
Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na makampuni na vyombo vya habari, ana haki ya
kupatiwa taarifa yoyote inayodhikiliwa na Serikali au na taasisi au
shirika lolote la serikali katika ngazi zote, kama taarifa hiyo
inahitajika kwa ajili ya maslahi ya uwajibikaji kwa umma. Zaidi ya hayo,
kila mtu, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Zimbabwe, ana haki
ya kupatiwa taarifa inayoshikiliwa na mtu yeyote, pamoja na Serikali,
kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya kufurahia au kulinda haki
yake. Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Katiba Mpya ya Kenya nayo pia imetoa
uhuru mpana wa habari kwa wananchi wa Kenya.
Kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni fedheha kwamba nchi yetu iliyokuwa ya
kwanza kupata uhuru katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini
inaelekea kuwa ya mwisho katika masuala ya uhuru wa habari kwa watu
wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM
kulieleza Bunge lako tukufu ni lini italeta muswada wa sheria kwa lengo
la kufuta urithi huu wa fedheha wa sheria za kikoloni ili Tanzania
iendane na karne mpya ya uhuru wa habari na wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa vyombo vya habari vya Serikali yaani, Radio na Television za
Taifa ndio vinatoa matangazo kwa wananchi kuhusu kile kinachoendelea
Bungeni. Kwa bahati mbaya ni kwamba Radio ya Taifa ambayo inasikilizwa
na watanzania wengi wa hali ya chini na kati katika maeneo mengi ya
mijini na vijijini wanashindwa kusikiliza mijadala inayoendelea Bungeni,
kwani matangazo yanakatishwa pindi kipindi cha maswali na majibu
kinapomalizika. Matangazo ya mjadala wa Bunge yanaendelea kurushwa
kwenye Television ya Taifa hadi Bunge linapoahirisha shughuli zake kwa
siku.
Mheshimiwa Spika,
Huku ni kutowatendea
haki watanzania wengi kwa kuwapa fursa kusikiliza nini wawakilishi wao
wanachokiongea katika mijadala mbalimbali Bungeni. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona sasa ni muda mwafaka kwa sekta binafsi nazo kufanyakazi
hiyo ambayo inaonyesha imevielemea vyombo hivyo vya serikali na kuondoa
ukiritimba uliopo wa kurusha matangazo ya Bunge.
3.2 Matangazo ya serikali kwenye vyombo vya habari
Mheshimiwa Spika,
Suala la matangazo ya serikali katika vyombo vya habari si kwamba
limekuwa likitumika kuminya uhuru wa habari katika baadhi ya vyombo vya
habari hususan vinavyoonekana kuwa vinafanya utafiti katika habari zake
kwa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na hivyo kuweka
hadharani mapungufu na uchafu wa Viongozi waliopewa dhamana na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Suala hilo la matangazo
badala ya kuviimarisha vyombo vya habari ili viweze kusimama na
kufanyakazi bila ya kuingiliwa, sasa linatumika kama njia ya kufifisha
uhuru wa kutafuta na kutoa habari na kuvifanya vyombo vya habari
kuachana na uhandishi wa uchunguzi na hivyo kukiuka haki za walaji za
kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya katiba ya 18 (d).
Mheshimiwa Spika,
Sasa kumezuka mtindo mwingine wa kuhamishia raslimali za Serikali
kwenye chama kwa ajili ya kuiokoa CCM na wanasiasa wengine. Tutatoa
mfano hai wa hivi karibuni kabisa. Kwa wafuatiliaji wa habari katika
vyombo vya habari, bila shaka watakumbuka kuwa siku ya Mei Mosi, Gazeti
la CCM linaloitwa Uhuru, lilikuwa na kurasa 79, ikiwa ni ongezeko la
karibu mara tatu ya gazeti hilo linavyotoka kwa siku za kawaida kama
halina matangazo.
Kinachoweza kuwa kimewasikitisha wafuatiliaji
makini wa masuala ya habari ni kwamba matangazo hayo hayakuwa ya watu
au kampuni binafsi yalikuwa ni matangazo ya serikali na taasisi zake,
kwa maana ya kwamba yaligharimu mamilioni ya shilingi za walipa kodi wa
Tanzania, ambayo kimsingi yalipotumika ‘hovyo’ kama tutakavyoonesha kwa
hoja hapa;
Mheshimiwa Spika,
Tatizo hapa si tu
kwamba gazeti hili ni la CCM, bali pia kuna masuala ya msingi kadhaa
ambayo kwa kweli mtu yeyote makini, anayejua biashara ya matangazo, hasa
kutangaza kupitia vyombo vya habari, anapaswa kuzingatia mara zote
kabla hajaamua kutumbukiza mamilioni kwa ajili ya kujitangaza;
Kwanza, kama chombo hicho ni gazeti, basi linapaswa kuwa na wasomaji
wengi na pia mzunguko mkubwa sokoni kwa maana ya kuwafikia watu wengi
kutokana na kusambaa maeneo mengi ndani (na nje ikibidi) ya nchi.
Mfuatiliaji yeyote makini wa vyombo vya habari anajua wazi kuwa gazeti
hilo la CCM, halina sifa hizo.
Kama serikali na taasisi
zilizotumia gazeti hilo la CCM kama njia ya kujitangaza zingekuwa makini
na matumizi halali ya fedha za Watanzania, lazima zingezingatia kanuni
za kawaida kabisa; yaani kuhakikisha wanapata wasomaji na soko kubwa
katika bidhaa na huduma zao wanazotangaza, hivyo wangepaswa kutangaza
katika magazeti yanayosomwa na yenye mzunguko mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Kinachoonekana hapa ni kwamba, baada ya njia nyingine za kifisadi za
kupata fedha kuisaidia CCM kushtukiwa, sasa zimebuniwa mbinu nyingine za
kifisadi za kusaka fedha kwa ajili ya chama hicho, mojawapo ikiwa ni
hii ya utoaji wa matangazo kwa vyombo vya habari vya CCM, visivyokuwa na
sifa stahili. Haya ni matumizi mabaya ya matangazo yenyewe na fedha za
umma!
Ni namna ile ile ya kutoa zabuni kwa Kampuni ya CCM, ifanye
upanuzi wa eneo la bandari kwenye eneo la CCM, bila makampuni yenye
uwezo kushindanishwa ili kupata moja iliyo makini na yenye vigezo vya
kufanya kazi husika.
3.3 TCRA NA UANGALIZI WA VYOMBO VYA HABARI VYA KIELEKTRONIKI
Mheshimiwa Spika,
TCRA ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya elkroniki kama Radio
na Televisdion, lakini imeshindwa kabisa kusimamia vyombo hivyo
walivyovipatia leseni ya kufanyakazi, kwani baadhi ya vituo ukisikiliza
vinafanya uchochezi wa kisiasa, kidini, ukabila wa wazi lakini vimeachwa
hadi matatizo ya udini yaliposhika kasi ndio Serikali ikaanza kukimbia
kuchukua hatua.
Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa
intaneti haitawaliwi na sheria yoyote nchini, baadhi ya vipindi vya
redio na televisheni havizingatii maadili ya Kitanzania, maeneo mengi ya
vijijini hayana huduma ya televisheni. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema
kuwa huu ni udhaifu wa wazi kwa mamlaka hiyo iliyopewa jukumu la
kusimamia. Hivyo basi tunaitaka Serikali itoe kauli kuhusiana na
udhibiti wa TCRA katika suala hilo.
ka 2013)
3.4 SHIRIKA LA UTANGAZAJI TANZANIA (TBC)
3.4.1 TBC na matukio muhimu ya Kitaifa
Mheshimiwa Spika,Ikiwa
imepita takribani miaka mitano tangu Mhe. Raisi alipozindua rasmi
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) mwezi mei 2008. Kwa kuwa, pamoja na
uchakavu na ukosefu wa vifaa TBC imeweza kupanua masafa yake ya
utangazaji karibu nchi nzima ,na kwa kuwa hili ni shirika la umma, ni
matumaini makubwa kwa watanzania kuwa TBC ingekua mstari wa mbele katika
kuripoti na kutangaza matukio muhimu yanayoendelea katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa TBC imekua nyuma katika kuripoti matukio muhimu
na badala yake imekua ikiweka vipindi visivyoendana na matukio
yanayolikabili taifa. Hii ni dharau kwa watanzania wengi hasa
ukizingatia kuwa hili ni shirika la umma na si la mtu binafsi hivyo
wajibu wake mkubwa ni kumpa taarifa mtanzania kwa wakati hata pale
inaposhindwa kutoa taarifa ama kuwepo eneo la tukio basi lazima programu
zake ziendane na hali halisi.
Mheshimiwa Spika, Kwa
masikitiko makubwa wakati wa ajali ya meli ya MV Skagkit iliyotokea
mwaka jana, 2012, wakati kuna taarifa za awali za ajali, TBC ilikua
ikiweka na kupiga muziki wa taarabu bila ya kuzingatia uzito wa ajali
ile, hata siku iliyofuata kwa ajili ya shughuli za uokoaji TBC
iliendelea kuweka programu ambazo hazikuendana na uzito wa tukio lile
licha ya kuwa mamia ya watanzania walipoteza maisha na huku tafrani
ikizuka kwa baadhi ya watanzania ambao ndugu zao walikua katika tukio
lile.
Mheshimiwa Spika,Katika kuonesha kuwa TBC
haijifunzi kutokana na makosa, ama labda imekosa uongozi wenye weledi na
umakini tangu kuisha kwa ajira ya mkurugenzi wao makini Tido Muhando,
mwezi wa April 2013 ambako kulikua na mlipuko wa bomu Arusha,tukio
ambalo lilikuwa kubwa kwenye historia ya nchi yetu kwani ni mara ya
kwanza tukio kama hilo kutokea, TBC iliendelea na urushaji wa matangazo
na vipindi tofauti huku televisheni na vituo vingine vya binafsi
vilikuwa vinajulisha taifa kuhusiana na tukio hilo.
Mheshimiwa Spika,
Tukiwa katika mijadala ya muhimu ya mustakabali wa taifa letu, ambapo
tunajadili na kupitisha bajeti kwa ajili ya watanzania, TBC hukata
matangazo ya vipindi vya Bunge wakati uwasilishaji wa hoja muhimu
ukiendelea. Wakati wa hotuba ya Mambo ya ndani, wakati msemaji mkuu wa
kambi ya upinzani anakaribia kuanza kusoma maoni ya Kambi ya Upinzani ,
TBC walikata matangazo na kuweka sherehe za Mwenge.
Mheshimiwa Spika,Pamoja na hayo yote, TBC bado inaendelea na kauli mbiu yake ya 'Ukweli na Uhakika'
kauli ambayo haiendani na uhasilia wa uratibu wa vipindi vyake vya
matangazo na uwasilishaji wa taarifa kwa umma. Mara nyingi kwenye
mijadala na hoja nzito ambazo Serikali inakua ina hali mbaya, matangazo
ya bunge hukatwa kwa kisingizio kuwa mitambo au matatizo ya kiufundi
yametokea, mbona matangazo au hitilafu za ufundi hazitokei katika
sherehe za Mwenge?Ama hitilafu kwenye kuonesha ujio wa rais wa China ?
TBC inatumika na imeendelea kutumiwa na Serikali ya CCM katika kuminya
haki ya mtanzania ya kupata habari si kwa sababu ya ufinyu wa bajeti
peke yake bali kuwaridhisha watawala. Lazima TBC ibadilike na kujua kuwa
ina dhamana katika kupeleka habari na taarifa sahihi kwa umma kwa
wakati na si kwa kuendeshwa kama roboti.
4.0 MASUALA YA VIJANA
4.1 UUNDAJI WA BARAZA LA VIJANA LA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
suala la mchakato wa uundwaji wa Baraza la Taifa la Vijana, sasa
umekuwa si tu wimbo bali zimwi la muda mrefu linaloiandama serikali ya
CCM na imeshindwa kabisa kuepukana nalo.Sera ya zamani ya maendeleo ya
vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na
suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali
imekuwa ikiwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa
yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa
maendeleo ya vijana nchini. Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba
katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vyama mbalimbali viliahidi
kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa linaundwa.
Mathalani, CHADEMA katika Ilani yake 2010-2015 kipengele 6.4.1 (viii)
ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai
wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya
CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo
limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.
CCM nayo
kupitia ilani yake ya katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa
vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha
uanzishaji wa Baraza la Vijana”.Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani
inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika suala hili la kuanzishwa
kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja kuisimamia
Serikali itekeleze Sera na ahadi badala ya kuitetea kwa udhaifu
iliyouonyesha.
Mheshimiwa Spika; Katika Hotuba ya
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Wizara ya Habari, Utamaduni na
Michezo juu ya mapitio ya utekekelezaji kwa mwaka 2010/2011 na makadirio
ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/2012 tulihoji ni lini hasa
Serikali ingewezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani ilirudia tena kuhoji suala hili wakati wa
mjadala wa mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2011/2012 na makadirio ya
mapato na matumizi kwa mwaka 2012/2013. Hata hivyo, kwa nyakati zote
hizo Serikali katika majumuisho imekuwa irudia tena ambayo imekuwa
ikitolewa kwa miaka zaidi ya miaka 17 ya kukamilisha mchakato wa
kuanzishwa kwa baraza la Vijana la Taifa; bila utekelezaji kamili na wa
haraka.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inayo
taarifa kwamba kufuatia hali hiyo mwezi Januari 2013 mbunge wa Ubungo,
Mheshimiwa John Mnyika aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge muswada binafsi
wa sheria kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Taifa la Vijana. Katika Hotuba
yake juu ya mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2012/2013 na makadirio ya
mapato na matumizi ya mwaka 2013/2014 ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kiongozi
wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Freeman Mbowe alihoji ni lini Serikali
itawasilisha bungeni miswada binafsi ya wabunge ukiwemo muswada huo.
Mheshimiwa Spika;
kwa mujibu wa Kitabu cha hoja za wabunge na majibu ya Serikali kuhusu
Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kwa mwaka wa
fedha 2013/2014 juu ya muswada huo “Ofisi ya Katibu wa Bunge
imemwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata ufafanuzi kama Muswada
unaohusu uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa hautakuwa na athari
zozote za kiwango cha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kama
ilivyoanishwa katika Kanuni ya 95 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la
mwaka 2007”.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inayo taarifa kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri kuwa
muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa
umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi. Kambi Rasmi ya
Upinzani ina taarifa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri
huo kwa kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu
cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa
madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango
ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya
vijana.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza iwapo katika kutoa ushauri huo ilizingatia
kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili cha muswada huo kinataja vyanzo
mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko
zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya
Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.
Mheshimiwa Spika;
Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka kuwa “fedha ambazo
hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile zote ambazo
zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe
kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka ufafanuzi kutoka kwa Serikali ni kwanini
haikutoa ushauri wa kufanya ibara hiyo ya Katiba ya Nchi kutumika
kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho
kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya
mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba
jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe
limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”
Mheshimiwa Spika;
Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa Kifungu cha pili kinataja mambo
yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja na muswada wa sheria kwa
ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana
na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko mwingine wowote au
kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote isipokuwa
kupunguza”. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka 17 maraisi na mawaziri wenye
dhamana wamekuwa wakiacha kutumia madaraka hayo ya kikatiba kuleta
muswada bungeni wa kuwezesha kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa;
hivyo kitendo cha Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu kuendeleza
vikwazo hata kwa muswada binafsi wa mbunge kuhusu suala hilo kunaashiria
ukosefu wa nia njema kwa upande wa Serikali katika mchakato wa kuundwa
kwa Baraza la Vijana la Taifa.
Mheshimiwa Spika; Kambi
Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Serikali na Uongozi wa Bunge
kuwezesha muswada wa Baraza la Taifa la Vijana kuwasilishwa kwenye
mkutano huu wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea iwe ni kupitia muswada
binafsi, muswada wa kamati au muswada wa Serikali kwa kuwa tayari maoni
yameshakusanywa kwa miaka mingi kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa
Sera na ahadi.
Kambi rasmi ya upinzani, Tunataka kujua msimamo
wa Serikali katika bunge hili, ituambie muda mahsusi (time frame) lini
hasa mchakato wa uundwaji wa baraza hilo utakamilika na hatimaye kuanza
kufanya kazi kwa Baraza la Vijana la Taifa kwa ajili ya maslahi ya
vijana wa nchi hii. Iwapo Serikali ya CCM itaendelea kupiga dana dana
muswada wa sheria wa kuundwa kwa chombo hiki muhimu kwa maendeleo ya
vijana; Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA
itawahamasisha vijana nchi nzima kuelekeza nguvu na uwingi wao katika
kuishinikiza Serikali sikivu ya CCM, kufanya mabadiliko yenye kuwezesha
matakwa ya vijana kutekelezwa kwa wakati.
4.2 Sekta ya maendeleo ya vijana
Mathalani katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka jana, kazi pekee ambazo
zimekuwa zikipewa kipaumbele na sekta hii ni kukimbiza mbio za mwenge
na kuratibu maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa. Aidha kwa mwaka jana,
sekta hii, kwa mujibu wa maelezo ya wizara, ilifanya uratibu wa mafunzo
ya kuwawezesha vijana kuwa na mawazo ya kimkakati ya ubunifu na
ujasiriamali katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Mara, Morogoro, Geita,
Njombe, Kigoma na Arusha!
Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka
wizara kulieleza bunge lako hili kwa takwimu na maelezo ya kina ni kiasi
gani mbio za Mwenge ambazo zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha
‘kuingiza’ mamilioni ya fedha, zimeweza kuwasaidia vijana wa Tanzania
kupambana na tatizo kubwa linalowakabili la ukosefu wa ajira na ujira
wenye staha. Je, wizara inaweza kutoa takwimu hapa kuonesha namna
ambavyo mabilioni ya fedha waliyotengewa mwaka jana kwa ajili ya uratibu
wa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali, wameweza kufundisha vijana
wangapi na katika maeneo yapi hasa ya utaalamu na taaluma, kwa kiwango
gani ili kuweza kuwajengea uwezo wa kuajiriwa na kujiajiri kwa ajili ya
kupata ujira wenye staha.
4.3 Mikataba, mipango, sera na utekelezaji
Mheshimiwa Spika,
Mwaka mzima baada ya serikali kusimama hapa bungeni na kulipatia bunge
lako matumaini na kutoa ahadi kemkem wakati wa kupitisha Azimio la
Mkataba wa Kimataifa wa Vijana wa Afrika, hadi sasa wizara hii
imeendelea kusuasua na kuzidi kutoa ahadi juu ya ahadi kuhusu kuweka
utaratibu wa kisheria wa utekelezaji wa mkataba huo.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya bunge hili katika mkutano wake wa mwezi Februari mwaka jana
kupitisha azimio hilo, katika hotuba ya bajeti mwaka jana, wizara hii
ilisema kuwa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
imeanza kuchukua hatua za kuandaa muswada wa sheria ya utekelezaji wa
mkataba huo.
Mheshimiwa Spika, Lakini katika kuonesha
kuwa serikali hii haikuwa wala haina nia ya dhati kuweka utaratibu wa
kisheria ili kusaidia utekelezaji wa azimio hilo, katika malengo yake ya
utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2013/14, imeshindwa
kabisa kuzungumza chochote juu ya suala hilo.
Kambi rasmi ya Upinzani,
inaona kuwa huu ni mwendelezo tu wa serikali hii ya CCM kuendelea na
utamaduni wake wa kuwatelekeza,kuwapuuza na kuwadharau vijana wa nchi
hii.Aidha , tunataka kujua ni lini wizara italeta mswada huo hapa
Bungeni kwa ajili ya kupitishwa na Bunge na kuwa sheria.
4.4 Mbio za Mwenge wa Uhuru
Mheshimiwa Spika,mara
kadhaa sasa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji maswali
anuai kuhusu jambo hili lakini bahati mbaya yamekuwa yakitolea majibu
yasiyokidhi haja. Nasi kwa ajili ya kutimiza wajibu wetu wa kuwasemea
Watanzania wasiokuwa na sauti ndani ya mhimili huu, tutaendelea
kukumbushia na kuhoji hadi majibu mujarabu yakakapotolewa.
Mathalani, katika moja ya malengo ya utekelezaji wa mpango wa bajeti wa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ukimbizaji wa Mwenge
wa Uhuru. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, si tu kwamba imekuwa ikihoji
maana nzima ya kuendelea kutumia mabilioni ya walipa kodi maskini kwenye
mbio za mwenge, badala ya kuuweka makumbusho na kuufanya kuwa moja ya
vivutio vya kiutamaduni.
Mheshimiwa Spika, mtu yeyote
makini hawezi kuona mantiki ya mbio za mwenge ambazo zimekuwa zikitumia
mabilioni ya fedha kuzunguka nchi nzima kuzindua miradi ya mamilioni ya
watu binafsi! Kama vile bar, nyumba za kulala wageni na mingineyo.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka huu wa fedha tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya
kukimbiza mwenge, randama ya wizara inaonyesha kuwa ,kijifungu 210319
zinaombwa shilingi 3,000,000 ‘kwa ajili ya kulipa matibabu na bima kwa
wakimbiza Mwenge wa uhuru’,kijifungu 210315 zinaombwa shilingi
64,200,000 ‘kwa ajili ya kulipa posho za kujikimu kwa wakimbiza mwenge
wa uhuru, kijifungu 220302 zinaombwa shilingi 57,750,000 ‘kwa ajili ya
kununulia dizeli ya magari mawili yatakayotumika kwenye sherehe za
uzinduzi na kilele cha mbio za mwenge wa uhuru’,.
Aidha,
kijifungu 220604 sare, wizara inaomba kiasi cha shilingi 8,886,000 ‘kwa
ajili ya sare za wakimbiza Mwenge kitaifa’, kijifungu 220708 zinaombwa
shilingi 25,000,000 ‘kwa ajili ya kukodi ndege kwa shughuli za mbio za
Mwenge wa uhuru’, kijifungu 220709 ,zinaombwa jumla ya shilingi
7,200,000 zinaombwa kwa ‘ajili ya ununuzi wa vifaa vya mkutano wa
tathimini ya mbio za mwenge wa uhuru’,kijifungu 221005 zinaombwa
shilingi 78,500,000 ‘kwa ajili ya posho ya safari za kikazi ndani ya
nchi kwa wakimbiza mwenge kitaifa’ ,kijifungu 221406 zinaombwa shilingi
15,000,000 kwa ajili ya ‘...kuandaa tuzo ...wakati wa mbio za mwenge’,
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kutengwa kwa fedha zote hizi kiasi cha shilingi 259,536,000
pesa ambazo zingewekezwa kwenye mfuko wa kuwakopesha vijana zingeweza
kuwakwamua kwenye tatizo la ajira, serikali inaomba fedha hata kwa ajili
ya kukodi ndege kwa ajili ya kukimbiza mwenge , mwaka huu tutashuhudia
mwenge ukikimbizwa angani! bado mwenge umeendelea kupoteza mwelekeo
Mheshimiwa Spika, katika kuthibitisha kuwa Mwenge umepoteza mwelekeo katika mwaka huu wa fedha katika kijifungu 230600 ‘matengenezo ya mashine’ katika kijifungu 230605 ‘mikataba ya matengenezo kutoka nje’ randama uk.86 inasema ‘mwaka
2013/2014 sh.366,000 zinaombwa kwa ajili ya kupata wataalamu nje ya
wizara kwa ajili ya kutoa huduma ya matengenezo ya chombo cha Mwenge wa
uhuru’. Unaweza kuona kuwa chombo hiki kinatafutiwa mtaalamu
kutoka nje ya wizara na malipo ya mtaalamu huyo ni shilingi laki tatu!
Hii ni dalili ya wazi kuwa chombo hiki yafaa kikawekwa kwenye jumba letu
la makumbusho.
Kambi Rasmi ya Upinzani, haikubaliani na serikali
kutumia kiasi cha shilingi 259,536,000 kwa ajili ya posho za kukimbiza
mwenge, tunataka fedha hizi ziingizwe kwenye programu za maendeleo ya
vijana ili waweze kujiajiri na mwenge uwekwe kwenye jumba la makumbusho,
kwani umekuwa ni kero kwa wananchi vijijini kuchangishwa fedha za
mwenge bila hata kujua zinaenda kufanya nini.
5.0 USIMAMIZI WA MICHEZO NA MUSTAKABALI WAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na hazina ya wanamichezo nchini, lakini michezo mingi nchini
haipewi kipaumbele na serikali.Mara kadhaa vyombo vya habari vimekua
vikiupa kipaumbele mchezo wa soka kana kwamba michezo mingine haina tija
kwa taifa. Leo hii kuna michezo ambayo kama ikipewa uzito wa kutosha
italeta taifa hili heshima katika medani za kimataifa.
Mheshimiwa Spika,Labda
kwa kuwa tumeshindwa kuwekeza kwenye michezo mingine kwa vipaumbele
ambavyo vinaweza kuiweka Tanzania katika ramani ya michezo, hii imefanya
michezo hiyo kufa na hazina ya taifa ya vipaji mbalimbali nayo kufa
bila kutumika. Mfano katika michezo ya 30 ya Olimpiki iliyofanyika
jijini London, Uingereza Julai mwaka 2012, Tanzania ilipeleka jumla ya
wanamichezo 7 ambao hawakuambulia medani yoyote .
Mheshimiwa Spika,Wakati
Afrika ya Kusini ilipeleka wanamichezo 125 kwa jumla ya michezo 17,sisi
tulipeleka 7 tu. Kuna jambo kuu la kujifunza kutokana na jinsi ambavyo
Serikali, sikivu , ya CCM inaendesha nchi yetu. Jambo ambalo
linastaajabisha na lenye maswali mengi yasiyo na majibu, Je Wizara hii
ina kazi gani? Ina mikakati gani ya jumla katika kusimamia vyama vya
michezo nchini ili viwe na tija? Je wizara hii ina uchungu na fedha za
kodi za wananchi hii kwa matumizi yasiyo na tija katika sekta ya
michezo? Je taifa hili limekosa kutumia michezo kama njia mojawapo ya
kutangaza jina la Tanzania na kuliweka katika ramani ya dunia kwa kuwa
na wanamichezo bora na si bora wanamichezo?
Kambi rasmi ya
Upinzani, inapendekeza kwa msisitizo mkubwa kuwa katika kipindi hiki
ambacho taifa letu lipo katika mpasuko na mgawanyiko wa masuala
mbalimbali kuanzia udini,mchakato wa katiba nk , katika kipindi hiki
ambacho mshikamano na umoja wetu kama taifa upo katika hatari ya
kusambaratika, jambo ambalo linaweza kutuunganisha kama taifa moja
lililobakia ni michezo .
Hivyo basi tuhakikishe kwamba timu
ya taifa ya mpira wa miguu inaandaliwa vya kutosha na tuweze kuingia
kwenye fainali za kombe la dunia ifikapo 2014, tuna kazi ndogo ya
kuifunga Morocco kwao, tunatakiwa kuifunga Ivory coast hapa kwetu,
tunaamini inawezekana kama mipango madhubuti ikiwekwa sasa.
5.1 Chama cha Riadha Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2012, katika mashindano ya taifa ya riadha kulikua na changamoto
kubwa ya wanariadha kushiriki katika mashindano ya taifa bila ya
maandalizi ya kutosha, huku baadhi ya wanariadha wakishiriki katika
mashindano bila ya kuwa na viatu. Haya ni mashindano ya taifa, Chama cha
Riadha (RT)nchini, kimeyandaa bila ya kuwa na mikakati ya kitaifa ya
kuhakikisha kuwa vigezo na viwango vimefuatwa.
Aidha , chama hiki
kimekuwa kikilalamikiwa sana na wadau wake kutokana na hisia kwamba
kunakuwa na upendeleo katika kutuma wanariadha ambao wamekuwa
wakiwakilisha taifa letu katika michezo mbalimbali ya kimataifa.
Kambi rasmi ya upinzani,
inataka kujua serikali imechukua hatua gani dhidi ya viongozi wa chama
hiki ambao badala ya kusimamia riadha wamekuwa hawafanyi hivyo , aidha
kuna mikakati na mipango gani ya kuinua kiwango cha riadha hapa nchini
ili kurudhisha heshima ya taifa kwenye mchezo huu maarufu duniani kote?
5.2 Mapato ya viwanja vya Taifa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama uk 102 katika mapato kuna kifungu 140259 ambacho
kinahusu mapato ya viwanja vya michezo (uhuru na Taifa) makadirio
yalikuwa kukusanya shilingi 400,000,000 kwa mwaka 2012/2013 ila
mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na asilimia 15 ya mapato yote
yanayokusanywa kutokana na kutumika kwa kiwanja hicho mpaka februari
2013 yalikuwa 329,814,400 tu.
Kambi rasmi ya upinzani,
inataka kujua mapato hayo yalikusanywa kutokana na michezo mingapi na
fedha hizo zilitumika katika kufanya kazi gani za kuendeleza michezo
hapa nchini.
5.3 Malipo kwa makocha wa kigeni.
Mheshimiwa spika,
katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni
1.230 katika kifungu 6004-280518 (Baraza la Michezo la Taifa –Makocha)(chanzo:randama, jedwali namba 8) kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC),Aidha kwenye fungu hilo hilo 6004 kwenye matumizi ya kawaida (chanzo randama ;jedwali namba 6) zimetengwa jumla ya shilingi milioni 586,079,000 kwa ajili ya mishahara na matumizi mengineyo zimetengwa shilingi 1,917,960,000
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya wizara uk.93 kijifungu 270800 ‘ruzuku kwa asasi na vituo’ zimetengwa jumla ya shilingi 1,564,382,000 na katika kijifungu kidogo cha 270813 ‘Baraza la Michezo la Taifa’ zimetengwa shilingi 1,524,382,000 kwa ajili ya ‘mishahara ya Makocha wa Kigeni’
na matumizi ya Baraza la michezo la Taifa. Aidha katika mwaka wa fedha
2012/2013 kwenye kijifungu hiki zilitengwa jumla ya shilingi 823,546,000 tu kwa ajili ya mishahara kwa makocha wa kigeni.
Wakati kichwa cha habari cha kasma hii na kijifungu hiki kikisema ni
‘ruzuku kwa asasi na vituo’ , ruzuku inayokwenda kutolewa ni kiasi cha shilingi milioni 40 tu
kama ambavyo inaonekana kwenye kijifungu 270839 kituo cha michezo
Arusha shilingi milioni 20 na kijifungu 270840 kituo cha michezo Songea
shilingi milioni 20.
Kambi rasmi ya upinzani, inaona
kuwa fedha hizi ni nyingi sana kwa ajili ya mishahara na marupurupu ya
makocha wa kigeni, hivyo basi tunataka kujua yafuatayo;
i. Ni makocha wangapi watalipwa na ni wa michezo gani?
ii. Wanapewa marupurupu gani kama stahili zao?
iii. Kwanini serikali na wizara hii isiwapeleke makocha wa kitanzania
mafunzoni nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi wakimaliza
masomo yao?
6.0 BARAZA LA KISWAHILI TANZANIA
Mheshimiwa Spika,Wizara
inao wajibu wa kuimarisha, kukuza na kuendeleza lugha yetu ya Kiswahili
kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano ikiwa ni pamoja na uratibu na
kuhakikisha ustawi na maendeleo ya utumiaji wa Kiswahili kwa
kushirikiana na asasi zile ambazo zinahusika na uendelezaji wa lugha hii
hapa nchini. Baraza lina wajibu wa kuhakikisha kuwa matumizi ya
Kiswahili yanapewa kipaumbele katika maisha ya kila siku ya mtanzania,
ikiwemo katika shughuli za kitaifa na kimataifa ambazo viongozi wa taifa
letu wanahudhuria.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na nyimbo ambazo
Serikali ya CCM imekua ikiziimba mara kwa mara kuwa inataka kukuza
lugha ya Kiswahili ili kuutangaza utamaduni wa Tanzania katika jumuia ya
kimataifa ni aibu kubwa kwa taifa letu pale ambapo viongozi wake
waandamizi wanapokuwa watumwa wa lugha za nchi za Magharibi!
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa Serikali ya CCM imeamua kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na
nchi ya China, ni kitendo cha kusikitisha na aibu kuona kuwa wakati wa
ziara yake nchini, Raisi wa China, alihutubia na kuzungumza kwa ufasaha
lugha ya taifa lake wakati Rais wa Tanzania na Waziri wa Mambo ya nje na
ushirikiano wa kimataifa wakitumia lugha ya Kiingereza. Swali la
kujiuliza, kama Raisi wa nchi pamoja na waziri wake wanaona ugumu
kutumia lugha ya taifa wakati mgeni wao ametumia lugha ya taifa lake
wakati walengwa wa ujio ule na wageni wengi waliokuwa katika uzinduzi wa
Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wengi walikua ni watanzania, je
itakuaje kwa mwananchi wa kawaida leo? Lugha ya Kiswahili haiwezi kukua
wala kupewa umuhimu na mataifa mengine ikiwa viongozi wa Serikali
wanaonesha hadharani utumwa wa utamaduni wa nchi za magharibi, lazima
kwa nguvu zote Bunge na taifa tukatae aina hii ya utumwa kwa maana kuwa
hata Serikali inayotakiwa kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili na
kukitangaza, wamekua mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani
tunajiuliza hivi, Hata kama Serikali ya CCM imeshindwa kulinda tembo
wetu basi hata Kiswahili mshindwe kukilinda? Tunarudia tena, huu ni
utumwa! Haukubaliki! Tutumie na kukitangaza Kiswahili kwenye dhifa na
hafla za kimataifa, kwa kuwa Kiswahili ndiyo urithi wetu.
7.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII NA USHIRIKI WA SERIKALI KATIKA UTEKELEZAJI
Mheshimiwa Spika,
Sheria ya hakimiliki inayotumika sasa katika kusimamia hakimiliki na
hakishiriki za wasanii , ni sheria iliyopitishwa na Bunge inayojulikana
kama Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya 1999. Hii iliiondoa
sheria ya awali Sheria ya Hakimiliki namba 61 ya 1966. Sheria hii
imeendelea kutumika baada ya kutungwa kanuni mbalimbali mwaka 2000 na
kuanza kutumika zikiwemo sheria iliyounda COSOTA. COSOTA ilianza kwa
kuwa na bodi iliyokuwa mchanganyiko wa wajumbe waliochaguliwa na wasanii
na wajumbe walioteuliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara. Na hali hii
ya kuwa na wawakilishi wasanii katika COSOTA iliendelea mpaka baada ya
uchaguzi mkuu wa chama hicho 2007, ambapo Waziri hakuweza kuteua
Mwenyekiti wa bodi ya chombo hicho na hivyo kuzuia Bodi kuweko.
Mheshimiwa Spika,hata
alipoulizwa na Mh. Martha Mlata kwenye bunge la bajeti 2008 aliahidi
kushughulikia na hakufanya hivyo hata akaulizwa tena bunge la bajeti
2009. Hivyo hatimaye 2011 ikateuliwa Bodi ambayo haikuwa na muwakilishi
kutoka wasanii japokuwa COSOTA iliendelea kukusanya mirabaha ‘kwa niaba
ya wasanii’.
Kambi rasmi ya upinzani, inataka kujua ni kwanini
bodi hii haina mwakilishi wa wasanii kama sheria inavyotaka? Lini
mwakilishi huyo atateuliwa na wizara?
7.1 Kulinda kazi za wasanii
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2001, ilitengenezwa kamati iliyoitwa National Anti Piracy
Committee ikiongozwa na Mwenyekiti John Kitime, iliyokuwa chini ya
COSOTA, kazi yake kubwa ni kuwezesha kutengeneza sheria na kanuni za
kuwezesha kazi za audio na video kuwa na stika za mapato. Kazi hii
ilifanyika na kukamilika na kanuni hizo zilipita kwa usimamizi wa Waziri
Mh. Juma Ngasongwa kabla tu ya uchaguzi wa mwaka 2005, lengo likiwa ni
kupata sapoti ya wasanii.
Mheshimiwa Spika, Baada ya
jitihada za hapa na pale, Serikali kwa kupitia TRA wameleta stika mpya,
ambazo Tatizo moja tu hapa ni kuwa TRA kazi yao ni kukusanya kodi tu na
sio kulinda hakimiliki, hivyo stika ya TRA ni stika ya kukusanya kodi na
italeta mkanganyiko katika utekelezaji wa taratibu za hakimiliki. Je,
wizara imepanga mikakati gani kuhakikisha kuwa kazi za sanaa
hazidurufiwi, kuuzwa na kusambazwa bila ya ridhaa za wasanii nchini?
Kambi rasmi ya upinzani bungeni inarudia kuitaka Serikali kuifumua
COSOTA na kuunda chombo kipya kitachokuwa na uwezo wa kusimamia kazi za
sanaa.
7.2 Nyimbo za wasanii na Mapato kwao.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2003 zilipitishwa kanuni zilizoagiza wenye vyombo vya utangazaji
nchini ziwalipe wanamuziki kutokana na matumizi ya nyimbo zao mbalimbali
ambazo wanazitumia kwenye vipindi mbalimbali. Ni jambo la kushangaza
kuona kuwa Serikali ya CCM inayojitapa kuwa na utawala wa sheria
inashindwa kudhibiti vyombo vya habari na utangazaji ambavyo vimeendelea
kutumia kila aina ya ubabe na njia za kiunyonyaji ili visilipe fedha
hizi kwa wasanii. Leo hii wasanii wanalazimishwa kuandika barua kuwa
wametoa nyimbo zao kwa vyombo hivyo zipigwe bila kulipia na kutokana na
mazingira yaliyotengenezwa, wanamuziki wanajikuta ni lazima wahonge! ili
nyimbo zao zipigwe ili waweze kupata soko la kazi zao.
Mheshimiwa Spika,Wizara
hii ambayo inasimamia TBC, televisheni na redio ya Taifa, imeshindwa
kuvichukulia hatua za kisheria vyombo vyake ambavyo vimekua moja wapo ya
wakiukaji wa sheria hii. Ni kejeli kwa taifa, ni kejeli kwa wasanii
wanaopata shida kujikwamua kimaisha. TBC leo inapiga na kucheza nyimbo
za wasanii bila kuwalipa, huku wizara inayotakiwa kusimamia vyombo hivi
inashuhudia sheria zilizopitishwa na bunge hili zinavunjwa.
Mbaya
zaidi TBC inauza CD na kanda za nyimbo zilizoko katika maktaba yake bila
kutoa hata senti kwa wanamuziki waliorekodi nyimbo hizo, iko wapi
tofauti yao na maharamia wengine? Leo hii wizara inawezaje kusema kuwa
wao ni wasafi? Ni aibu kwa wizara, ni aibu kwa watendaji wake, ni aibu
kwa serikali , sikivu, ya CCM!
7.2 Harakati za kudai haki za wasanii.
Mheshimiwa Spika,
sanaa imeendelea kufanywa mtaji wa biashara na watu wachache ambao
wanatumia nguvu waliyo nayo katika jamii na uwezo wao wa kifedha katika
kukandamiza maslahi ya wasanii hapa nchini. Katika harakati za kutafuta
haki za wasanii hapa nchini, mimi binafsi pamoja na wasanii wengine
wachache, tulianzisha harakati za kudai haki kwa kupitia programu
maarufu iliyojulikana kama 'Anti Virus' chini ya 'Vinega'
ikiwa na lengo na juhudi za kudai haki za wasanii dhidi ya ukandamizaji
unaofanywa na wajanja wachache kwenye muziki, ambao wametumia nafasi
kama njia ya kutumia mitaji yao ya fedha kuwaendesha wasanii jinsi
wanavyotaka wao.
Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kawaida,
wasanii wengi walidharau jitihada zetu na kutotuunga mkono. Leo hii
katika tasnia ya muziki, kuna mgogoro mkubwa uliofuka moto kati ya
msanii maarufu Lady Jaydee dhidi ya wamiliki wa radio ya Clouds FM hatua
iliyosababisha nyimbo za wanamuziki wa kizazi kipya maarufu kama 'Bongo Flavour'
kutopigwa kwa siku moja katika kituo hicho. Sasa, ukiangalia kilio cha
Lady Jaydee ni kilio kilekile kilichopelekea VINEGA kuingia vitani.
Mheshimiwa Spika,
kama msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, na mwenye dhamana na
uchungu na tasnia ya sanaa nchini, niweke wazi kwa umma wa watanzania
kuwa, tumefikia hapa tulipo si kwa kuwa na sheria kandamizi tu bali pia
kwa kukosekana kwa umoja wa wasanii nchini. Wakati tukiwa na juhudi za
kutetea maslahi ya watanzania kupitia Anti Virus, ni wasanii
wachache ambao walituunga mkono na wengi wao wakibeza jitihada zetu,
wakiwemo hawa ambao leo wanalalamika kuwa wananyonywa haki zao. Wengine
walifikia hatua ya kusema kuwa tumepewa fedha ili kuzima harakati
tulizozianzisha.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa wasanii hasa wa
muziki wa kizazi kipya nchini, unasimamiwa na chombo halali
kinachojulikana TUMA-‘Tanzania Urban Music Association’, lakini kutokana
na ujanja wa watu wachache, waliudhoofisha umoja huu kwa kuanzisha
kampuni iliyosajiliwa kama TFU- ‘Tanzania Flavour Unit’ iliyowalaghai
wasanii kuwa ni muungano wa wanamuziki wa Bongo Fleva na kuhodhi
majukumu ya TUMA ambacho ni chama halali cha kusimamia wanamuziki wa
Bongo Fleva. Mpaka tunapoongea leo hii, hata Studio iliyotolewa na
Mheshimiwa Raisi, bado ipo katika mikono ya TFU pamoja na Serikali
kuamuru irudishwe katika mikono ya Serikali ili ikabidhiwe kwa wasanii
wote chini ya chama halali cha TUMA. Sasa tunataka wasanii wote nchini
waache uoga na unafiki na wajiunge na vyama vyao halali ili viwatete
haki zao.
Mheshimiwa Spika,Kumekuwa na upotoshaji mkubwa wa
utetezi wa haki za wasanii kwa kuwa wanaotuhumiwa kunyonya haki za
wasanii wameweza kutajirika na kuneemeka kwa kupitia jasho na mgongo wa
wasanii. Hawa hawa wanaotuhumiwa kuhujumu wasanii ndio wanatumia nafasi
yao kuupotosha ukweli wa tuhuma dhidi yao. Wanatumia fedha na rasilimali
walizo nazo katika kunyanyasa wasanii, kuwakandamiza, kuwapokonya haki
zao na kuwadhalilisha kuwa bila wao, wasanii wasingekua kitu.
Mheshimiwa Spika,
Leo hii wasanii wanaishi kwenye hali ngumu, umasikini mkubwa lakini
bado wanatolewa maneno ya kashfa na dharau na Serikali imeendelea kukaa
kimya. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka Serikali kuacha siasa
kwenye kutatua migogoro ya taifa hili. Siasa zimetumika sana katika
kuzima jitihada za wanyonge kwenye taifa hili, leo hii wananchi hawana
imani na Serikali kwa kuwa imeonesha wazi imeshindwa! Kushindwa kwa
Serikali katika kutatua migogoro ya wasanii kwa kutotekeleza makubaliano
mbalimbali yanayoafikiwa kati yake na wasanii, yameshusha hadhi yake
kwa wasanii. Swali kubwa kwa Serikali sikivu ya CCM, Je mnasubiri
migogoro mingapi ili mjue kuwa wasanii hawatendewi haki? Je mnasubiri
vikao vingapi vya upatanishi na usuluhihishi ili mjue kuna tatizo? Ama
mnataka wasanii wagombane, wapigane, wauane ili mjue kuwa kuna tatizo?
Mheshimiwa Spika,Leo
hii, Serikali bila ya kukaa na wadau wa muziki wa dansi, taarabu, bongo
fleva, hip hop, mnanda na mahadhi mengine na kuwasikiliza kwa makini
wamejikuta wanajihusisha na mambo ambayo hawajui. Watendaji wa Serikali
wameendelea kuwaingiza mkenge viongozi wa Serikali katika masuala ya
sanaa nchini. Hivi karibuni,hapa Dodoma, bila ya kuwa na taarifa muhimu
juu ya unyonyaji wa haki za wasanii, waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda,
alishiriki katika tamasha la kudai haki za wasanii ambalo liliandaliwa
na baadhi ya watu ambao kwa muda mrefu wamekua wakituhumiwa kuwa ni
wanyonyaji wa kazi za wasanii. Kiongozi mkuu wa Serikali, unashiriki
katika kupiga mihuri na kuhalalisha mikakati ya kimafia ya kuua umoja wa
wasanii bila ya kuwa na taarifa sahihi. Je, waziri mkuu ana taarifa
kuwa walioandaa tamasha la kudai haki za wasanii ndio walalamikiwa namba
moja nchini dhidi ya haki za wasanii hasa wa muziki? Tuinataka Serikali
na wanasiasa wote kuacha kutumia wasanii kwa faida zao binafsi bali
wasaidie kutatua matatizo halisi ya wasanii ili waondokane na umasikini.
8.0 UTAMADUNI NA MALIKALE NCHINI
Mheshimiwa Spika,Zipo
njia mbalimbali ambazo zinatambulisha utamaduni wa mtanzania kwa
mataifa mengine. Utamaduni wetu unatambuliwa kwa kupitia lugha, mavazi,
vyakula, sanaa, maadili na malikale za taifa letu. Leo hii ukiangalia
makumbusho ya taifa, haina vitu vya msingi vya kufanya makumbusho kuwa
chanzo cha kuliingizia taifa fedha za kigeni kwa njia ya utalii. Sehemu
nyingi nchini ambazo zinaelezea utamaduni wetu na asili ya taifa letu,
kama Bagamoyo, Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje, Isimila, Zanzibar haziwekwi
katika mazingira ya kuyatunza kwa ajili ya kuelezea asili ya taifa letu.
Leo hii , Serikali ya CCM ikijitetea kuhusu kuboresha ama kutunza
malikale za taifa letu ikiwemo majengo ya kale, itajigamba kuwa
imeyapaka rangi. Lakini ni maajabu kuona majengo yale, yamepakwa rangi
nyeupe, chokaa hali inayoyafanya majengo haya kuwa na rangi za kijani
zenye ukungu inapokuja suala la ukarabati wake. Ukiangalia marekebisho
ya majengo hayo, yamefanyika na kuondoa uasilia wa majengo hayo kama
yalivyokua zamani,.
Kambi rasmi ya Upinzani, inaiuliza
Serikali je,imeshindwa kutafuta wataalamu wa majengo wenye kuweza
kurekebisha na kuyatunza majengo katika hali ilokuwa bila ya kuyaharibu
zaidi? Ni mikakati ipi ambayo Serikali imejiwekea kwa mwaka huu wa fedha
wa 2013/2014 katika kuyatunza na kuyatengeneza majengo ya kale ili
kutunza utamaduni wa taifa letu?
10.0 UCHONGAJI WA VINYAGO NA THAMANI YAKE KWA TAIFA
Mheshimiwa Spika,Kama
kawaida Serikali ya CCM imeendelea kutawala huku kukiwa hakuna
utaratibu mzuri wa kusimamia maslahi ya wachongaji wa vinyago hapa
nchini. Wachongaji wa vinyago ambao wamesaidia kwa kiasi kikubwa
kutangaza utamaduni wa taifa letu kwa kutumia kazi zao za sanaa hapa
nchini hasa katika kutangaza utalii.
Kwa taarifa tulizonazo kutoka
kwa wachongaji vinyago ni malalamiko ya kazi zao za sanaa kununuliwa na
kisha kusafirishwa kuelekea nchi za nje ambapo huko hupigwa mihuri kuwa
imetoka katika nchi za jirani. Hii imeua soko la vinyago hapo nchini na
kukandamiza maslahi ya wachongaji hawa ambao ni hazina kwa taifa letu.
Wachongaji vinyago wana umuhimu mkubwa katika kulinda utamaduni wa nchi
yetu kwa kuwa ni urithi tuliopewa na ni lazima Serikali iweke mikakati
ya kuhakikisha kuwa soko la vinyago ndani na nje ya nchi linamufaisha
mchongaji kimapato.
Kambi rasmi ya upinzani bungeni, inaitaka
Serikali kutoa kauli hapa bungeni ina mkakati gani uliowekwa kwa mwaka
huu wa fedha katika kuhakikisha kuwa wachongaji vinyago wananufaika kwa
kazi zao hasa ukizingatia kuwa, soko la ndani la vinyago halina faida ya
kutosha na usimamizi wa kina. Vinyago ambavyo vinachongwa Tanzania
vimeendelea kuuzwa nje ya nchi na kuzipatia nchi hizo mapato makubwa na
baadhi ya kazi hizo hazitambuliwi kuwa zinatoka nchini.
11.0 USIMAMIZI WA HAKI ZA WASANII KATIKA UUZAJI WA MIITO YA SIMU
Mheshimiwa Spika,Biashara
ya miito ya simu, inayofanywa na makampuni ya simu nchini ni biashara
ya siri ya kimafia inayohitaji kuwekwa wazi kwani kuna ukwepaji mkubwa
wa kodi na haki za wasanii, ambapo pamoja na waliojiunga kihalali
kutopata haki yao wako wale wanaokuta nyimbo zao zinatumika bila kujua
zimepelekwa huko na nani na kwa mikataba ipi. Leo vyombo vyote vya
Serikali vinavyotakiwa kusimamia sheria na kanuni za hakimiliki zinakaa
kimya huku wasanii wakipokwa haki zao, taifa likipoteza mapato na
kuubariki wizi huu wazi wazi.
Mheshimiwa Spika,Hivi karibuni
tumeshuhudia Serikali ya CCM kupitia wizara yake yenye dhamana ya
kufuatilia biashara ya miito ya simu, wizara ya mawasiliano, sayansi na
teknolojia imeshindwa kutoa majibu ya ufuatiliaji wa tozo na mapato ya
miito ya simu, Mmeshindwa kutimiza wajibu wenu kwa wananchi lakini pia
mmeshindwa kutimiza wajibu wenu katika kutekeleza matakwa ya katiba ya
nchi hii, kuulinda uhuru na haki za wananchi wake kama ambavyo muasisi
wa taifa hili alijitahidi kufanya.
12.0 TASNIA YA FILAMU NA MCHANGO WAKE KATIKA KUKUZA UCHUMI NCHINI
Mheshimiwa Spika,Tasnia
ya filamu nchini imeendelea kukua kila siku huku kukiwa na usimamizi
mdogo wa Serikali katika kuhakikisha kuwa sekta hii inatumika vizuri
kama chanzo cha kukuza ajira nchini lakini pia kama moja ya njia ya
kuwaongezea wananchi kipato na Serikali kukuza uchumi kwa kupitia kodi
mbalimbali. Leo hii, soko la filamu nchini Nigeria limeweza kuingiza
takribani kiasi cha dola 250 milioni kwa mwaka kama mapato ya filamu
zinazotengenezwa kwa soko lao la Nollywood, je Serikali kupitia wizara
hii imefanya tathmini gani kwa kupitia mamlaka za mapato na kujua soko
la filamu kwa mwaka linaingiza kiasi gani hapa nchini? Kambi rasmi ya
Upinzani, inaitaka Serikali ya CCM kuacha kufanya kazi kwa mazoea sasa
na badala yake ivisimamie vyombo husika kuhakikisha kuwa sekta ya filamu
inapewa kipaumbele pia na thamani ili kuweza kukusanya kodi na
kupunguza umasikini nchini. Tasnia ya filamu si tu inaweza kuliingizia
soko hili fedha bali pia ikipewa thamani inauwezo mkubwa kwa kutatua
tatizo la ajira hapa nchini. Kwa kuwa mpaka sasa, Tanzania imeshatoa
filamu nyingi na soko lake kupanuka katika nchi za Afrika Mashariki na
kati, je tasnia hii mpaka sasa imeweza kuzalisha ajira ngapi? Kambi
rasmi ya upinzani, inaitaka wizara kuja na takwimu rasmi za ajira
zilizotokana na tasnia hii kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Mheshimiwa Spika,Tanzania
ambayo imebarikiwa kwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo
Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro, Manyara,
Mikumi pamoja na hifadhi za wanyama kama Selous, Tarangire, maziwa
makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, sehemu zenye asili ya utumwa
kama Bagamoyo, Zanzibar, Kilwa Masoko, misitu mikubwa, mito na vivutio
mbalimbali; ina nafasi kubwa ya kutumika kama moja ya 'film
destinations' duniani kama ambavyo nchi nyengine imewekeza.
Mheshimiwa Spika,Nchi
mbalimbali zimeweza kujiingizia fedha za kigeni kila mwaka kutokana na
kutumia vivutio walivyo navyo na mandhari ya nchi zao kupitia tasnia ya
filamu. Nchini Afrika Kusini, tasnia ya filamu ina thamani ya kiasi cha
takribani randi 12 bilioni sawa na shilingi trilioni 2.17 za kitanzania
huku ikichangia kiasi cha shilingi 1.4 bilioni kwenye uchumi wa taifa na
ongezeko la kiasi cha shilingi milioni 400 kwa mwaka katika kipindi cha
miaka minne toka mwaka 2008 walipoamua kufanya mabadiliko ya tasnia ya
filamu. Zaidi , tasnia ya filamu imeweza kuongeza soko la ajira kwa
kutoa karibu ajira 30,000.[1]Afrika
kusini imeweza kutumia sekta hii kwa kwa kutumia mandhari waliyo nayo
ambayo inafanana na mandhari za takribani nchi 57 ulimwenguni na
kutumika kutengeneza filamu zenye mafanikio Hollywood. Ipo haja ya
wizara hii kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii kufanya
tathmini ya kina na kutengeneza mazingira ya kutumia vivutio tulivyo
navyo ili kuifanya Tanzania sehemu bora zaidi Afrika kwa ajili ya
kutengeneza filamu kwa kupitia mandhari zake. Lazima Serikali itengeneze
mkakati endelevu wa kuendeleza sekta ya filamu nchini kwa kuitangaza
Tanzania katika anga za kimataifa kama 'film destination' bora zaidi
Afrika.
13.0 MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
katika makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hii kwa mwaka wa fedha
2013/14, jumla ya shilingi 21, 328,045,000, zimeombwa kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Aidha, kama ilivyo ada
ya miaka yote kwa bajeti za serikali hii ya CCM, katika wizara zote,
fedha za matumizi ya kawaida ni nyingi kuliko fedha ambazo zinatarajiwa
kutumika katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Suala
linaloweza kumuumiza mdau yeyote ambaye angependa kuona wizara hii
ikisonga mbele ni pale ambapo miradi ya maendeleo imetengewa sh.
600,000,000 pekee, wakati kuna kiasi cha takriban bilioni 10 zimetengwa
kwa ajili ya kitu kinachoitwa ‘matumizi mengineyo’.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inahoji hayo matumizi mengineyo yasiyojulikana au kuelezwa hapa mbele
ya bunge lako lakini yanatengewa karibu nusu yote ya bajeti ya matumizi
ya kawaida, ni nini na yapi?
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
.............................. .........
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo.
20.05.2013
Post a Comment