UCHAGUZI WA ARUSHA WAAHIRISHWA TENA ILI KUIMARISHA HALI YA AMANI NA UTULIVU
Written By Unknown on Friday, July 5, 2013 | 18:28
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha tena uchaguzi wa madiwani kata nne za Arusha hadi Julai 14 kuruhusu kurejea utulivu baada ya mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa kampeni wa Chadema ulioathiri uchaguzi huo wiki iliyopita. Bomu hilo lilirushwa Juni 15 na mtu asiyejulikana katikati ya mkutano wa Chadema katika viwanja vya Soweto, mjini Arusha na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa na uchaguzi huo wa Juni 16 kulazimika kuahirishwa. Baada ya tukio hilo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Arusha aliuahirisha hadi Juni 30, lakini jana Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema utafanyika Julai. Kata zinazohusika ni Elerai, Kimandolu, Thani na Kaloleni. Akizungumza na waandishi wa habari, Jaji Lubuva alisema walipotangaza kuwa uchaguzi ungefanyika Juni 30 waliamini kuwa hali ya utulivu na amani ingekuwa imetengemaa. “Lakini kwa bahati mbaya tumejiridhisha kuwa hali bado inahitaji kuangaliwa kuhakikisha imerejea katika utulivu wake kikamilifu. “Hiyo haimaanishi kuwa ni mbaya, isipokuwa tumeona bado tunahitaji muda wa kama wiki mbili hivi kuona vumbi lililokuwa likitimka limetulia,” Jaji Lubuva alisema. Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, wapiga kura hawapaswi kutekeleza haki yao ya kupiga kura katika wasiwasi hivyo ni wajibu wa Tume kuhakikisha unaondoka na wapiga kura wanatekeleza haki yao kwa amani. “Tunataka watu wajihisi huru wakati wa kupiga kura, ndiyo maana tumeahirisha uchaguzi wa kata hizo kwa mara nyingine. Wanapokuwa na amani na uhuru wapiga kura wanaweza kuchagua wanayemtaka kwa utaratibu mzuri, vinginevyo, shughuli yote ya kupiga kura inaweza kuharibika,” alisema Lubuva. Aidha, alitaka wagombea na vyama kutoendeleza kampeni kwa sababu kuahirishwa kwa uchaguzi hakumaanishi kuwaongeza muda wa kujinadi au kutafuta wapiga kura wa kuwaunga mkono. “Muda wa kupiga kura haujabadilika. Vituo vya kupigia kura havijabadilika na vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10 jioni. Waliokuwa katika mstari ndio watakaopiga kura na watakaofika vituoni baada ya muda huo kwisha hawataruhusiwa kupiga kura ili kutoa nafasi ya kura kuhesabiwa,” alisema. Jaji Lubuva alisema matokeo ya uchaguzi huo mdogo yatatangazwa mapema na taratibu za uchaguzi zitazingatiwa ili kutoa haki kwa wapiga kura na wanaopigiwa kura. Inadaiwa bomu hilo lililokuwa kwenye mfuko wa plastiki, lilirushwa na mtu asiyejulikana. Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Amir Ally (7), Judith Moshi na Amir Ally.
Labels:
HABARI
Post a Comment